Balozi wa Japan Mheshimiwa Masaki Okada (wa kwanza kushoto) akiwa na Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli (nyuma ya Balozi) pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Usafirishaji nchini Rwanda Bw. Guy Kalisa (mwenye tai nyekundu) wakikagua eneo la kituo cha pamoja cha ukusanyaji ushuru kwa upande wa Rwanda. (HD)
Balozi wa Japan nchini Tanzania Mheshimiwa Masaki Okada ameelezea kuridhishwa na utekelezaji wa mradi ujenzi wa daraja la kimataifa la Rusumo na kituo cha pamoja cha ukusanyaji ushuru katika eneo la Rusumo mpakani wa Tanzania na Rwanda. Miradi hiyo miwili mikubwa inayofadhiliwa na Serikali ya Japan ilianza kujengwa mwezi Machi mwaka huu wa 2013 na imepangwa kukamilika mwezi Novemba mwaka 2014.
"Nimeridhishwa na viwango na kasi ya utekelezaji wa mradi huu" alisema Balozi Okada wakati alipotembelea eneo hilo la mpakani mwa Tanzania na Rwanda ambapo alisisitiza kuwa, inatia moyo kuona fedha zilizotolewa na nchi yake zikitumika vizuri kwa lengo la kukamilisha miradi hiyo kwa wakati.
Naye Meneja wa Tanroads wa Mkoa wa Kagera Injinia John Kalupale akitoa taarifa kwa Balozi huyo wa Japan ambaye alifuatana na Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, alielezea kuwa uamuzi wa kujenga daraja jingine katika eneo hilo la mpakani, unatokana na mahitaji halisi ya wakati huu kwani daraja linalotumika hivi sasa lilijengwa miaka 40 iliyopita likiwa na uwezo wa kubeba tani 32. Aliendelea kueleza kuwa ingawa miaka ishirini baada ya ujenzi wa daraja hilo kulifanyika ukarabati mkubwa kwa lengo la kuimarisha uwezo wake, bado kumeendelea kuwepo kwa ongezeko kubwa la magari hasa yanayosafirisha bidhaa kati ya Bandari ya Dar es Salaam na nchini jirani ya Rwanda.
Injinia Hitoshi Kamega ambaye ni Mhandisi Mkazi wa Kampuni mbili zilizoungana kuusimamia mradi huo ambazo ni Chodei Co. Ltd. na Nippon Koei Co, amelezea kuwa ujenzi wa daraja hilo la Rusumo lenye urefu meta 80 pamoja na kituo cha ushuru, unatekelezwa na Mkandarasi Daiho Co. kutoka Japan kwa gharama ya Shilingi bilioni 31.736.
Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli hata hivyo alibainisha kujitokeza kwa mapungufu katika baadhi ya maeneo ya mradi huo ambayo wizara yake kwa kushirikiana na Ubalozi wa Japan hapa nchini wanayafanyiakazi ili kuhakikisha kuwa kunakuwepo na uwiano mzuri wakati wa utekelezaji wa mradi huo na pale huduma zenyewe zitakapoanza kutolewa..
Waziri Magufuli aliyataja baadhi ya mapungufu hayo kuwa ni pamoja na kutotengwa kwa eneo la kutosha la maegesho ya magari kwa upande wa Tanzania na kuhitajika kwa upanuzi wa majengo ya huduma za kiutawala hasa wakati wa kutekeleza mipango ya baadaye kwa kuzingatia ongezeko la shughuli za kibiashara linavyoonekana katika eneo hilo.
No comments:
Post a Comment